Mbunge wa Viti Maalum – Kundi la Wafanyakazi, Mhe. Lucy Mwakyembe, ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Afya kuanzisha tawi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zanzibar kwa lengo la kuboresha huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi wa visiwani humo.
Mhe. Mwakyembe alitoa ushauri huo tarehe 12 Mei 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema uwepo wa tawi la JKCI Zanzibar utasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wagonjwa wa moyo wanaolazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata huduma za kibingwa, hali ambayo mara nyingi husababisha gharama kubwa pamoja na usumbufu kwa wagonjwa na familia zao.
Aidha, amesisitiza kuwa upanuzi wa huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali ya nchi ni hatua muhimu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa wakati na kwa urahisi zaidi.
Mhe. Mwakyembe ameongeza kuwa kuanzishwa kwa tawi hilo kutasaidia kuimarisha sekta ya afya Zanzibar na kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi wengi zaidi.

Leave a Reply